Waziri nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Bi Celina Kombani amesema serikali imeanza mchakato wa kulipa madeni yote ya walimu yanayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 33.8.

Waziri nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Bi Celina Kombani amesema serikali imeanza mchakato wa kulipa madeni yote ya walimu yanayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 33.8.

Amesema kati ya fedha hizo  shilingi bilioni 32.4 zimekwishatolewa kwa  ajili ya kuwalipa walimu wa shule za msingi na shilingi bilioni 1.4 zimetengwa kulipa madeni ya walimu wa sekondari nchi nzima.
Bi Kombani alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema mzunguko wa zoezi la kulipa madai ya walimu utakamilika Oktoba 15 mwaka huu.

Ametaja baadhi ya madai hayo ya walimu kuwa ni pamoja na fedha za matibabu,likizo uhamisho,marekebisho ya mishahara pamoja na posho za kujikimu.

Katika hatua nyingine serikali imewapokea walimu wapya na kuwaingiza kwenye orodha ya malipo ya mishahara yaani payroll kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.

Mbali na kuwaingiza kwenye orodha ya malipo ya mishahara walimu hao pia watalipwa posho ya kuanza kazi ya siku saba,nauli na pia watajaziwa taarifa zao za kiutumishi mara moja.

——————————————-

Jeshi la wananchi wa Tanzania linatarajia kuongoza operesheni maalum yenye lengo la kusaka mabomu katika eneo la Mbagala kufuatia kulipuka kwa bomu mbagala kizuiani kulikosababisha vifo vya watoto wawili na kujeruhi wengine watatu.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa mkoa wa Dar-Es-salaam, William Lukuvi amesema kufuatia tukio hilo, serikali imeunda kikosi kazi maalumu ambacho kitaongozwa na jeshi la wananchi wa Tanzania ambalo litatumia wataalamu na vifaa maalumu kusaka masalia ya mabomu katika eneo hilo.

Mbali na jeshi hilo kikosi kazi hicho kitawajumuisha askari wa usalama wa taifa na askari wa jeshi la polisi.

Bwana Lukuvi amewaomba wananchi wa eneo la Mbagala kutoa ushirikiano kwa kikosi kazi hicho ili kufanikisha zoezi la ukaguzi wa eneo hilo.

Amewataka kuchukua tahadhari juu ya uchomaji moto taka, kwa kutenga eneo maalumu katika mitaa, na kusimamisha shughuli zinazohusiana na uchimbaji wa ardhi pamoja na kutoa taarifa polisi, mara waonapo vyuma wanavyovitilia mashaka.

Akizungumzia tukio la jana, bwana Lukuvi amesema mtoto Stellah Chawala, aliyelazwa katika hospitali ya Muhimbili tayari ameshafanyiwa upasuaji, lakini hali ya mtoto huyo si ya kuridhisha. Kwa upande mwingine familia ya mtoto Rajabu Said aliyefariki jana imefanya mazishi ya mtoto wao leo.
——————————————————

Vyombo vya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar vimeiomba serikali kuongeza uwezeshaji wa rasilimali kwa maafisa na askari wake ili waweze kudhibiti matukio ya kihalifu yanayojitokeza visiwani pemba.

Akizungumza wakati wa mkutano wa ulinzi na usalama ulioitishwa na mkuu wa jeshi la polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, Mkuu wa Brigedia Nyuki Brigedia jenerali Salum Mustaafa Kijuu amesema kuwa askari wa vyombo hivyo hawajashindwa kudhibiti hali ya uhalifu inayotokea kisiwani pemba bali wanachohitaji ni uwezeshaji wa kifedha kwa ajili ya kununulia mafuta ya magari kwa ajili ya kufanyia doria.

Amesema mara nyingi matukio ya uhalifu ukiwemo uchomaji moto nyumba hutokea nyakati za usiku na kwamba kama kutakuwa na mafuta ya kutosha askari watafanya doria ili kudhibiti hali hiyo.

Awali mkuu wa jeshi la polisi IGP Saidi Mwema alitaka kuwepo ushirikishwaji wa wananchi katika ukusunyaji wa taarifa za intelejensia zitakazosaidia kuwabaini wahalifu na kuwakamata .

Amesema wananchi wakishirikishwa katika hilo wataweza kusaidia udhibiti na ulinzi wa amani.

————————————————
Serikali ya Japan, imetoa msaada wa yeni milioni 171 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 2.4 za Tanzania kwa ajili kupambana na ugonjwa wa ukimwi hapa nchini.

Mkataba wa msaada huo umetiwa saini leo baina ya katibu mkuu wa wizara ya fedha na uchumi Ramadhani Khijjah na balozi wa Japan hapa nchini bwana Hiroshi Nakagawa.

Akizungumza mara baada hafla ya utiaji saini wa mkataba huo,bwana Khijjah amesema utasaidia kudhibiti na kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi hapa nchini.

Kwa upande wake, balozi Nakagawa amesema msaada huo ni nyongeza ya shilingi bilioni 3.2 ambazo Japan imetoa mwaka jana kwa ajili ya kuhamasisha mapambano ya ugonjwa huo.
—————————————————–

Watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi kufuatia kuhusika na tukio la ujambazi katika tawi la Benki la NMB Temeke jijini Dar-Es-Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-Es-Salaam, Kamanda wa kanda maalum ya polisi ya Dar-Es-Salaam Suleiman Kova amesema polisi walifanikiwa kuwatia mbaroni Dereva wa taxi ajulikane kwa jina la Shaffi Kombo, mwenye umri wa miaka 33, anayedaiwa kuwachukua majambazi hao mara baada ya tukio pamoja na Richard Albert mkazi wa kigogo mwenye umri wa miaka 30.

Sambamba na tukio hilo, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata majambazi wengine sugu wawili waliohusika katika tukio la ujambazi eneo la Magomeni wakiwa na silaha aina ya bastola yenye usajili namba 02970 pamoja na risasi tatu.

Katika hatua nyingine watu watatu wamekamatwa na vocha kadhaa za shilingi elfu tano za kampuni ya simu za mkononi vodacom, zenye thamani ya shilingi milioni 90 ambazo zinasadikiwa kuibwa nchini Afrika ya kusini ambapo vocha hizo hutengenezwa.

Inadaiwa kuwa watu hao  Sadiki Jediwa , Mkazi wa Tandale, Muhsini Amini  mwanafunzi wa chuo cha biashara na Rashid Maulidi  walikuwa katika harakati ya kuziuza kwa thamani ya shilingi milioni 45.
———————————————-
Jamii na taasisi mbalimbali zimetakiwa kujitokeza kuchangia mfuko wa udhamini wa elimu na mafunzo ya baharia ili kuinua tasnia ya ubaharia nchini.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Dk. Maua Daftari wakati alipokuwa akizundua mfuko wa udhamini wa elimu na mafunzo ya baharia pamoja na kuendesha harambee ya kuchagia mfuko huo.

Aidha naibu waziri huyo amekiri kuwa serikali inatambua umuhimu wa mabaharia hivyo wameanzisha mfuko huo ili kuwawezesha Watanzania ambao hawana uwezo wa kujisomesha kupata elimu hiyo kwa njia ya mkopo.

Kwa upande wake Naibu mwenyekiti wa bodi ya Mfuko huo Bernard Mbalaileki amesema kuwa makusudi ya  kuanzisha mfuko huo ni kupanua wigo wa tasnia ya ubaharia na kuwawezesha vijana wengi kujitokeza kusomea mafunzo hayo ili kuongeza pato la taifa pindi watakapopata ajira za ubaharia katika nchi mbalimbali.

Bw.Mbalaileki amesema kuwa mbali na mfuko huo kugharamia ada za wanafunzi utasaidia kununulia vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika maabara ya mafunzo pamoja na meli ya kujifunzia. 

Aidha ameongeza kuwa tayari chuo hicho cha ubaharia kinatoa mafunzo ya cheti, stashahada na kwa sasa wanatoa shahada ya juu na wanapokea wanafunzi kutoka mikoa yote nchini.

Chuo hicho cha ubaharia kilichoanzishwa mwaka 1978 kimeweza kutoa mafunzo yanayokidhi matakwa ya kimataifa ikiwemo unahodha wa meli za ngazi ya juu na uhandisi wa meli.
————————————————-

Taifa halina budi kuandaa viongozi wenye uwezo wenye upeo wa juu katika mambo mbalimbali wakaoweza kutoa maamuzi sahihi kwa manufaa ya umma na kuchochea kasi ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa mafunzo ya juu ya uongozi kwa wafanyakazi wa umma jijini Dar-Es-Salaam, Katibu Mkuu ofisi ya Rais, Michael Mwanda amesema viongozi wenye uwezo wa kuongoza vema ni lazima waandaliwe kwa kupewa mafunzo yatakayowasaidia kutimiza wajibu wao.

Aidha amesema mafunzo ya juu ya uongozi yatasaidia kuleta maboresho katika utoaji huduma kwa umma.

Bwana Mwanda amesema mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia na kimawasiliano yameifanya sekta ya umma kuwa na mwamko katika kufahamu namna viongozi wanavyotoa uamuzi wa masuala mbalimbali yanayowagusa maisha ya wananchi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa maendeleo ya rasilimali watu, ofisi ya rais na utoaji huduma kwa umma, Roxana Kijazi, ametoa changamoto kwa viongozi kuongeza ujuzi na maarifa katika kazi kupitia elimu, ili kufanya kazi kwa ufanisi.

Mafunzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya wiki moja yalihudhuriwa na watumishi mbalimbali toka serikalini yakiwa na lengo ya kuwajengea uwezo na kuleta maboresho katika utoaji huduma kwa umma.
————————————————

Wananchi visiwani Zanzibar wameshauriwa kuzingatia sheria na taratibu, ili kujenga utulivu utakaofanikisha zoezi la uandikishaji katika daftari la wapiga kura.

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, bwana Mohamed Aboud ametoa ushauri huo leo jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa akijibu swali la Mwandishi wa Habari, kuhusu hali ya uandikishaji wapiga kura katika daftari la kudumu visiwani Pemba.

Amesema  haoni sababu ya kuwepo vurugu vsiwani humo, wakati utaratibu wa kisheria upo ambapo mwananchi atakayenyimwa kitambulisho cha ukaazi, anaweza kudai haki hiyo mpaka Mahakamani.

Aidha Naibu Waziri huyo amesema siasa za chuki zimepitwa na wakati, ambapo
amewataka Wazanzibari kusahau yaliyopita na kushirikiana kidugu katika kuijenga Zanzibar mpya.

Zoezi linaloendelea la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura visiwani Zanzibar limeleta mtafuruku mkubwa, hali iliyosababisha dalili za kuhatarisha amani.
———————————————
HABARI ZA KIMATAIFA

Serikali ya IRAN imekiri kuwa na mtambo wa pili wa kurutubisha madini ya uranium.

Hata hivyo imesema mtambo huo ni maalum kwa ajili ya utafiti wa masuala ya kiafya ambao hauna tishio kwa usalama wa dunia.

Rais wa Iran Mohamood AHMEDINAJAD amesema hayo katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha nchini Marekani ambapo amekuwa akihudhuria mkutano wa 64 wa umoja wa mataifa mjini NEW YORK.

Iran ipo katika mzozo na baadhi ya nchi hususan za magharini kutokana na kupinga angalizo la shirika la nguvu za atomic duniani kuhusu kudhibiti kuenea kwa silaha za kinuklia duniani.  Nchi hiyo inaendelea na mpango wa kurutubisha madini ya uranium huku mataifa hayo yakihofu endapo Iran itahodhi silaha za nuklia.

Rais wa Marekani, BARACK OBAMA,ameitaka Iran kusema ukweli na kujirekebisha sasa ili maneno ya viongozi wa Iran kuhusu nguvu za nuklia yaweze kuaminika kwa  jumuiya ya kimataifa.
——————————————-

Wakuu wa nchi sihiri tajiri duniani wameendelea kukutana katika mji wa PITTSBURG katika jimbo la PENSYLAVANIA nchini MAREKANI ili kujadiliana hali ya uchumi duniani pamoja na namna ya kupunguza ongezeko la hewa ya karboni duniani bila ya kuathiri uchumi wao.

Hata hivyo mkutano huo ulitawaliwa na maandamano ya wananchi wanaopinga sera za nchi hizo tajiri dhidi ya nchi maskini.

Waandamanaji hao wamepambana na polisi kwa muda mrefu wakitaka kushinikiza mkutano huo ufutwe kwa kwa madai hauna maslahi kwa watu masikini dunia.
———————————————————
Maharamia wanaofanya utekaji wa meli katika pwani ya nchi ya SOMALIA,wamemuua nahodha wa meli moja ya mizigo iliyokuwa inataka kutia nanga katika bandari ya nchi hiyo baada ya nahodha huyo kukataa meli hiyo isipandwe na maharamia hao ambao walitaka kuipeleka nje ya bandari hiyo ili wakaiopre.

Hii ni mara ya kwanza kwa maharamia wa Somalia kufanya shambulizi la meli karibu na mjii mkuu wa MOGADISHU,kwa kawaida maharamia hao huvizia meli nje ya bandari hiyo kwenye eneo la ukanda wa kimataifa.

Hata hivyo shambulio hilo lilizimwa na wanajeshi wanaolinda amani kutoka nchi za AFRIKA pamoja na wanajeshi wanaotii serikali dhaifu iliyopo madarakani ambapo shambulio hilo karibu na makazi ya viongozi wa serikali limezua hofu juu ya usalama wa wananchi kwa ujumla.

Waziri wa shughuli za bandari ABDIASIS HASSAN alisema kwa kawaida jeshi la polisi la nchi hiyo lina kawaida ya kuzisindikiza meli hizo hadi nje ya bahari kama zinaondoka au kusizindikiza zikiingia lakini safari hii maharamia waliwahi kabla ya polisi kufika.
————————————————————–
Katika uchaguzi wa ujerumani ambao unatarajiwa kuwa na mchuano mkali kati ya chama cha CDU kinachoongozwa na kansela ANGELA MERKEL na kile cha SDP kinachoongozwa na FRANK WALTER STEINMEIER,hali bado haijajulikana kuhusu nani hasa atashinda uchaguzi huo.

Wagombea wote wawili walionekana wakijipitisha huko na huko kuuza sera zao ambapo chama cha CDU chenye mrengo wa kidini limedai kuwa kitahakikisha kuwa kiwango cha maisha ya wajerumani hakitashuka cchini ya uongozi wao huku wale wa SDP wakidai kuwa hataongeza kodi.

—————————————————–

Uwekezaji katika sekta ya usafiri wa anga nchini ni wa muhimu katika kuchochea uwekezaji kutokana na kuongezea mzunguko wa biashara pamoja na kukuza utalii na pato la taifa.

Hali ya upatikanaji wa urahisi wa usafiri kwa njia mbalimbali inatoa mwanya kwa miji kuweza kujipanua na kuvutia wawekezaji pamoja na uwepesi wa jamii kuweza kufikia soka la ajira lilipo hivyo kupunguza kiwango cha umasikini.

Kampuni ya kitanzania ya Connect Africa imeongeza chachu katika sekta ya usafiri wa anga kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo kati ya majiji ya kibishara na utalii nchini ya Mwanza na Dar es salaam kwa kuanzisha safari za ndege kupitia ndege yake ya Zara International aina ya Boieng 737 – 200 mara nne kwa wiki.

Baadhi ya wasafiri wa awali wa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria mia moja na arobaini wametoa maoni yao kuhusiana na kuanza kwa safari zitakazokuwa kila siku ya Jumatatu,Jumanne,Alhamis na Ijumaa wakionesha kufurahia kuongezeka kwa ushindani katika soko katika sekta hiyo.

Kampuni hiyo ya Connect Africa imesema iko mbioni kuongeza njia za safari kuanzia mwezi ujao kwa  safari za kati ya Dar es salaam na Arusha na Dar es salaam Johannesburg Afrika Kusini.

Hata hivyo changamoto kubwa kwa mashirika ya ndege nchini ni kupanua wigo wa safari katika mikoa yenye uhaba ama isiyokuwa kabisa na huduma za usafiri wa anga ili kuwa na mtandao mpana wa safari hizo. 
——————————————————–

Shirika la Viwango la Kimataifa ISO limeyataka mataifa yanayoendelea kuongeza juhudi katika kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutumia bidhaa bora, ili kuepuka madhara yanayojitokeza kwa kutumia bidhaa hafifu.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Shirika hilo Dk. Alan Morrison wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kutembelea maabara za Shirika la Viwango Tanzania TBS, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili hapa nchini.

Amesema wakati mataifa yanapambana na kuzagaa kwa bidhaa duni, wananchi wamekuwa waathirika wakubwa kutokana na bidhaa hizo kuuzwa kwa bei nafuu, lakini bila kuwa na ufahamu wa athari zinazoweza kuwapata.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TBS Bw. Charles Ekelege alimweleza Rais huyo wa ISO mipango ya shirika lake katika kukabiliana na uingizaji wa bidhaa duni, ikiwemo kufanya ukaguzi wa bidhaa katika nchi husika kabla ya kusafirishwa na kuingizwa nchini.

Amesema TBS pia inaendelea na mikakati ya kuwaelimisha wenye viwanda na wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora, ili kuhakikisha kwamba bidhaa za Tanzania licha ya kukidhi matakwa ya viwango, lakini pia zinakubalika kwenye masoko ya kimataifa.

Rais wa ISO ambaye alitarajiwa kukutana na Viongozi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko pia alishiriki tukio la kukabidhi vyeti na leseni za ubora, kwa wazalishaji waliokidhi vigezo katika kuzalisha bidhaa zenye viwango vya ubora.
—————————————————
Sekta ya utalii itaendelezwa endapo wadau mbalimbali wa sekta hiyo watapatiwa elimu ya kutosha itakayowasaidia kuboresha ufanisi katika kazi zao katika kutoa huduma mbalimbali zihusianazo na sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwakabidhi vyeti wahitimu wa mafunzo maalumu kwa walimu wa utalii nchini, Waziri wa Mali ya asili na utalii Shamsa Mwangunga amesema mafunzo hayo ni nyenzo muhimu ya kupanua wigo wa huduma na kuboresha sekta hiyo.

Amesema kufuatia ushindani unaoibuka katika soko la utalii sekta hiyo haina budi kuhakikisha inatoa wataalamu wenye kukidhi mahitaji ya soko ili kuvutia watalii nchini.

Mafunzo hayo ambayo yanatoa muongozo wa mitaala kwa vyuo vya fani ya utalii yanalengo ya kuvisaidia vyuo hivyo kutoa wataalamu watakao himili ushindani ulipo kimataifa katika fani hiyo.

Mafunzo hayo wamefadhiliwa na umoja wa ulaya ambapo jumla ya wahitimu 37 vikiwemo vyuo vya ufundi VETA vya mikumi na Dar-Es-Salaam, Njuweni na Victoria chuo cha utalii.
———————————————

Kampuni ya bia Tanzania TBL imekabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi kwa Jeshi la Polisi la kikosi cha Usalama barabarani kwa ajili ya maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo asubuhi jijini Dar es salaam katika Makao Makuu ya Kikosi hicho cha Usalama barabarani-Trafick baina ya Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TBL-Maneno Mbegu na Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani James Kombe.

Aidha vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja na fulana na stika zilizobeba ujumbe wa kauli mbiu ya wiki ya nenda kwa usalama unaosema Epuka Mwendo kasi kabla haujatuua,Usinywe Pombe na Kuendesha.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Meneja Uhusiano na Mawasiliano TBL Maneno Mbegu amesema kampuni hiyo inashirikiana na jamii ili kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inapatikana ili kuzuia ajali za kizembe.

Aidha Mbegu amewataka madereva kuwa waangalifu kwa  kuzingatia sheria za barabarani,ikiwa ni pamoja na kuacha kuendesha magari wakiwa wamelewa.

Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani James Kombe ameipongeza kampuni ya TBL kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanashikiana na jeshi hilo kutoa elimu ya usalama barabarani kwa raia,pia amewapongeza madereva wa mikoani kwa kuzingatia mwendokasi wawapo safarini.

Hata hivyo Kamanda Kombe amesema kuwa Jeshi lake halitayafumbia macho magari yote yanayotumia vifaa chakavu katika magari yao,hivyo kuwataka wamiliki wa magari kuwa na tabia ya kuyafanyia ukaguzi magari yao mara kwa mara.

Maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa usalama yanatarajiwa kuadhimishwa kuanzia tarehe 28 mwezi huu hadi tarehe 3 Oktoba,Mkoani Mbeya na inatarajiwa kuzinduliwa na Naibu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shamsa Vuai Nahodha.
—————– 

Tanzania itaungana na Mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya kichaa cha Mbwa Duniani, tarehe 28 Septemba mwaka huu , huku juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo hppa nchini zikiwa chini ya wastani ya ule unaopendekezwa na Shirika la afya duniani (WHO) na Shirika la Afya ya Wanyama duniani (OIE).

Akitoa taarifa ya serikali kuhusu maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. James Wanyancha, amesema katika miaka minne iliyopita kuanzia 2005 hadi 2008, kumekuwa na ongezeko la matukio ya ya watu wanaoumwa na Mbwa wenye kichaa na kusababisha baadhi yao kupoteza maisha.

Amesema kwa mfano mwaka 2005 watu walioumwa na mbwa 14,264 ambapo mwaka 2008 walikuwa 17,990, matukio ambayo yalisababisha vifo vya watu 120.

Aidha Dk. Wanyancha amesema serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Maliasili na Utalii na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa imechukua hatua za kuhamasisha wananchi madhara ya ugonjwa huo na namna ya kukabiliana nao pamoja na kutoa chanjo kwa mbwa na paka ili kudhibiti ugonjwa huo.

Madhimisho ya kitaifa ya kichaa cha mbwa yatafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro, ambapo pamoja na mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, inatekeleza mradi wa miaka mitano ya kudhibiti kichaa cha mbwa unaofadhiliwa na Taasisi ya Bill na Melinda Gates chini ya Uratibu wa WHO na serikali.
—————————————————————     
Watumishi wa umma wamekumbushwa kuwashirikisha wananchi katika kupanga na kutumia fedha za umma ili kuondoa manung’uniko katika jamii.

changamoto hiyo imetolewa na wanaharakati wa kudhibiti matumizi ya fedha za umma wa asasi ya dhahabu ya jijini dar es salaam.

Wamedai kuwa kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma imekuwa ni chanzo kikubwa cha  kulegalega kwa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Wamedai kuwa karibu nusu ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zimekuwa hazitumiki kwa malengo yaliyokusudiwa.

—————————————————

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: